FALSAFA YA KIAFRIKA
Falsafa
ni dhana ambayo haina namna moja ya kuifasili, wataalamu mbalimbali wametoa
mawazo yao kuhusu dhana hii ya falsafa.
Wamitila
(2003) anasema kuwa falsafa ni istilahi inayotumiwa kuelezea wazo au mawazo aliyonayo
mtu au mwandishi. Mfano falsafa ya mwandishi inaweza kulenga mawazo ya
mwandishi kuhusu maisha, mila, desturi, au utamaduni wa jamii husika atokayo
mwandishi.
Sadipo
(1993) anasema kuwa falsafa ni udadisi unaohusu dhana na kanuni zinazotuongoza
kuhusu uzoefu au mazoea kuhusiana na maadili, dini, sheria, saikolojia,
historia, sayansi za jamii, na siasa.
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa falsafa ni taaluma inayo dadisi hali halisi ya
maisha ya binadamu kwa kuzingatia imani, mila, desturi, pamoja na mienendo
aliyonayo binadamu katika jamii yake, huku akitafakari njia sahihi na bora za
kuweza kutatua changamoto mbalimbali anazo kabiliana nazo katika maisha yake ya
kila siku.
Kuhusu
falsafa ya kiafrika wataalamu kama vile Placide Temples (1959), Oruka (1990),
na Mbiti (2011). Wameifafanua dhana hii ya falsafa kuwa ni fikra au mitazamo wanayoishughulikia waafrika wenyewe au watuwengine ambao
wanakubali mila na desturi za kiafrika.
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa falsafa ya kiafrika ni dhana au mawazo ya waafrika
juu ya mambo mbalimbali wanayoyafanya kama vile imani waliyonayo juu ya maisha,
mila, desturi, namna ya kushirikiana katika katika jamii, na kutafuta suluhisho
juu ya changamoto au matatizo yanayowakabili.
Vilevile
kuna kuna sifa mathubuti zinazo itambulisha falsafa ya kiafrika, sifa hizo ni kama
vile; falsafa ya kiafrika imejikita katika tanzu za fasihi simulizi, mfano
visasili, visakale, sifo, ngano, mafumbo, vitendawili, miviga, ngomezi,
tambiko, na ngoma.
Fasihi
andishi; ni sanaa inayowasilishwa kwetu kwa maandishi. Hapa mkazo mkubwa hupo kwenye
lugha, maandishi, na nyezo inayotumiwa kuiwasilisha au kuyawasilisha maandishi
hayo. Fasihi andishi ni tokeo kuu la maendeleo ya jamii na kuvumbuliwa kwa
mfumo wa maandishi (Wamitila, 2004).
Ni
kweli kabisa kuwa falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika tanzu za fasihi
simulizi na andishi ya Kiswahili. Kwa kuanza na fasihi simulizi ya Kiswahili,
tanzu zifuatazo zinathibitisha hujidhihirishaji wa falsafa ya kiafrika miongoni
mwa tanzu hizo ni kama zifuatazo;
Falsafa
ya kiafrika inajidhihirisha katika hadithi; hadithi simulizi ni masimulizi
ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au
sahili (Wamitila, 2003). Kuna aina mbalimbali za hadithi simulizi kama vile
ngano, visasili, visakale, hekaya, na nyingine nyingi. Kwa kiasi kikubwa
falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika hadithi. Kwa mfano katika hadithi ya
Fumo Aliongwe au Liyongo Fumo,
“…Siku moja walikuwa msituni wakiwinda na
wanawe. Harafu wakapumzika. mwanawe
akamuuliza naye akatoa siri ya kifo chake. Alisema kuwa yeye asingekufa
isipokuwa kwa kudungwa kwenye
kitovu chake kwa sindano ya shaba…”
Kutokana
na hadithi hii ni dhahiri kuwa waafrika wanaamini nguvu uhai kama anavyodokeza
Placide Temples. Katika hadithi hii Fumo Aliyongwe aliweza kufa kirahisi baada
ya kutolewa nguvu uhai. Vilevile katika hadithi ya ‘Rwanda Magere’ tunaona kuwa
Rwanda Magere anategemea nguvu uhai zilizo katika kivuli chake. Hivyo kutokana
na hadithi hizo ni dhahiri kuwa falsafa ya kiafrika hujidhihirisha katika hadithi
simulizi.
Falsafa
ya waafrika inajitokeza kupitia ushairi wa fasihi simulizi, waafrika wana mfumo
maalumu wa fikra na hujishughulisha na mila, desturi, tamaduni, na namna ya
kutatua matatizo yao. Katika wimbo wa Tom Malanga ulioimbwa na bendi (kundi) la
Les Wanyika falsafa mbalimbali za kiafrika zimejidhihirisha kupitia wimbo huo.
Dai hili linathibitishwa katika ubeti wa tatu (3) unaosema;
“Tamaa ya maisha ndiyo chanzo cha maovu yote
duniani.
Tamaa ikizidi mwisho wake
husahau hata ndugu zako.
Sababu ya tamaa hujali hata
wazazi wako.
Mkeo na watoto umewaacha na
rafiki.
Sababu ya tamaa umesahau amri
za Mungu.
Kwamba usiue wala usiibe,
usitamani vya watu.
Waheshimu baba na mama yako.
Tamaa mwisho ni majuto Ee wacha tamaa”
Msanii
anadhihirisha waziwazi falsafa ya kiafrika anapozungumzia masuala ya ndoa,
saula la dini, suala la maadili na suala la malezi ya familia. Hayo ni masula
yaliyopo na yanayotokea katika jamii. Mwanafalsafa wa kiafrika “ Tempeles”
anasema falsafa ya kiafrika imejikita katika mila, desturi, na tamaduni za
kiafrika. katika wimbo huu kutokana na tamaa mbaya vijana wanakiuka maadili,
hawawajali wazazi wao, wamewaacha marafiki, ndugu, wake, na watoto pia. Sababu
ya tamaa wamesahau amri za mungu kuwa usiue. Usiibe, usitamani vya watu, pia
waheshimu baba na mama yako. Mwisho wa tamaa ni kifo na kupelekwa gerezani.
Hivyo basi msanii anaamini na anaonya kuwa mwisho wa tamaa ni majuto
tuache tamaa.
Falsafa
ya kiafrika katika semi, semi ni tanzu ya fasihi simulizi ambayo
hujishughulisha na maneno yasiyokua na majibu ya moja kwa moja kwa msikilizaji
ama hadhira. Katika utanzu huu kuna vipera vinavyo ambatana nacho, baadhi ya
vipera hivyo ni misemo, nahau, mafumbo, na lakabu. Semi ina dhima zake katika
jamii inapotumika na baadhi ya dhima hizo ni kama vile kuelimisha jamii juu ya
mambo mbalimbali mazuri ya kufanya, kama kufanya kazi kwa bidii, mfano msemo wa
“asiyefanya kazi na asile”. Pia semi
zina dhima ya kuonya na kuadabisha jamii juu ya mambo mbalimbali mabaya na
yasiyofaa katika jamii, kama wizi, imani na tabia mbaya, mfano msemo usemao “mkaidi hafaidi mpaka siku ya idi”. Semi
ni miongoni mwa tanzu za fasihi simulizi inayoonesha falsafa ya jamii moja na
nyingine. Wanafasihi wana dhihirisha kuwa falsafa ya kiafrika inaweza
kujidhirisha katika utanzu huu wa semi kwa kupitia vipera mbalimbali vya utanzu
huu. Kwa mfano, kupitia methali
mbalimbali zinazotumika katika jamii ya waafrika dai hili linaweza kuthibitishwa,kwa
kutumia mifano ya methali zifuatazo; “mwenye
nguvu mpishe”, “Aungurumapo simba mcheza nani?”, na “Nazi haishindani na jiwe”. Kupitia
methali hizi ni dhahiri kuwa falsafa ya Afrika inadhihirisha kuwa katika
masuala ya utawala, waafrika walikuwa katika makundi madogo madogo kama vile
koo au makabila, na mtu aliyekuwa anaaminika kuwa ni mwenye nguvu ndiye
aliyekuwa anatawala katika jamii husika. Viongozi waliokuwa wanaaminika kuwa ni
wenye nguvu ni kama vile; chifu Mkwawa, Kinjekitile Ngwale, na Chifu Mangungo
wa Msovelo.
Falsafa
ya kiafrika ikijidhihirisha katika sanaa za maonesho; katika kujadili vipengele
vya ujidhihirishaji wa falsafa ya kiafrika, tumechagua vipera viwili katika
utanzu huu ambavyo ni matambiko na ngoma.
Matambiko,
ni kipera cha sanaa za maonesho ambacho wahusika wake katika jamii hufanya
shughuli mbalimbali za kutoa sadaka kwa miungu, wahenga, na mababu
waliowatangulia, ambao wanaonekana wana nguvu asilia zinazosaidia kuepusha
utokeaji wa majanga kama njaa, radi, ukame, mafuriko, kuvamiwa au kutekwa kwa
utawala, pamoja na kushinda vita. Katika jamii ya wasukuma, matambiko mbalimbali
hufanywa ikiwemo matambiko yanayohusu kuzaliwa kwa mapacha (kulwa na doto) au
kuzaliwa kwa mtoto aliyetanguliza miguu badala ya kichwa kama ilivyozoeleka
(Ghashinje). Kwa upande wa mapacha wasipofanyiwa matambiko hatari inaweza tokea
kama vile mvua kugoma kunyesha, mapacha hao kupigwa na radi na pengine kufariki
dunia kabla ya kukua. Hii ina dhihirisha kuwa jamii ya wasukuma wanategemea
nguvu ya ziada katika kukabiliana na majanga. Kwa upande wa mtoto anayezaliwa
ametanguliza miguu, nae pia hufanyiwa matambiko ili aweze kuishi na kukua bila
kupata matatizo. Shughuli mbalimbali wakati wa matambiko hufanywa mfano ngoma,
nyimbo na sherehe zinazoambatana na wanyama kuchinjwa na damu zao kutumika kama
sadaka kwa ajili ya matambiko hayo. Katika kuthibitisha hili Placide Temples
anaeleza kuwa maisha ya jamii nyingi za wabantu wanategemea nguvu uhai (vital
force) ili kujikinga na utokeajia wa majanga katika jamii hizo kama
ilivyoneshwa katika jamii ya wasukuma.
Ngoma;
hiki ni kipera kinachoonesha utokeaji wa falsafa ya kiafrika katika maisha
halisi ya waafrika wenyewe. Ngoma katika jamii za kiafrika ni kiashiria cha
mambo muhimu, mfano hutumika kama nembo ya utawala, kitumbuizi katika shughuli
mbalimbali kama vile harusi au kupandishwa cheo. Katika jamii ya wasukuma ngoma
huwa ni za aina mbili. Kuna ile inayochezwa katika shughuli mbalimbali kama
vile harusi au matambiko na pia kuna ile ambayo inachezwa wakati wa kiangazi
ambayo huusisha pande mbili, upande wa kwanza wanajulikana kama Bhaghika na
upande wa pili ni Bhaghalu. Lengo kubwa ni kutumbuiza watu na kujua ubora wa
“Manju” katika ngoma hizo. Pia ngoma hizo zina pande mbili zinazoshindana na
hueandana na matumizi ya nguvu za asili (madawa ya kienyeji) ili kuwavutia
watazamaji na kumuona Manju wa upande gani atakuwa bora zaidi ya mwenzake.
Katika kujadili dhana ya falsafa ya kiafrika Temples anasema kuwa mwaafrika
hawezi kuacha asili yake ambayo ndiyo utambulisho wa utamaduni wake. Kama
ilivojidhihirisha katika jamii ya
wasukuma ngoma ni moja ya asili zinazotambulisha utamaduni wa jamii husika.
Baada
ya kuangalia falsafa ya kiafrika inavyojidhihirisha katika tanzu za fasihi
simulizi. Pia falsafa ya kiafrika inajidhihisha katika tanzu za fasihi andishi
ya Kiswahili kama inavyoelezewa katika vipengele vifuatavyo;
Falsafa
ya kiafrika inajidhihirisha katika ushairi; ushairi ni sanaa inayopambanuliwa
kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato,
picha au sitiari au ishara katika usemi, maandishi au maadhi ya wimbo (Mulokozi
na Kahigi, (1979). Kwa kutumia “Kunga za Ushairi na Diwani yetu” iliyoandikwa
na Kahigi na Mulokozi falsafa ya kiafrika inajidhihirisha kama ifuatavyo;
Waafrika
wanaamini katika suala la umoja; toka awali waafrika walikuwa na umoja waliishi
kwa kushirikiana na hata kufa nya kazi pamoja kwa manufaa ya jamii nzima. Kwa
kuumia shairi la “Msiba Uliotuangukia” suala la umoja kama imani ya waafrika
linajidhihirisha;
“…Na mara shambulio
tukalianza
Huko sauti za chuki
tunazipaza
Tobaa litumbo
la nduli kafiri
Atakaye
tumbole lituhasiri!
Tukalichoma
tukalikata sana…”
Shairi
hili linaonesha kuwa waafrika waliamini katika umoja kama nyezo ya kupinga
ukoloni na unyanyasaji. Pia waafrika wanaamini kuwa wazee ni watu wenye busara,
hekima, na mawazo mazuri ambapo ni vyema kuheshimu mawazo yao. Mfano katika
shairi lifuatalo;
“…Ndipo baina yetu utu umoja,
Mzee kidogo –
maisha meonja,
Kutunyamazisha
sote na kusema,
Tazama jama,
janga limetuponza!
Lakini hivi hivi kukaakaa,
Pasipo kujaribu
kujiokoa,
Ni jambo la
kijinga kupindukia…”
Suala
la kifo; vilevile waafrika wanaamini kifo sio mwisho wa uhai bali ndio mwanzo
wa maisha mengine. Waafrika wanaamini kuwa mtu akifa anaendelea kuishi kati yao
ingawa hawamuoni. Hii injidhihirisha katika shairi la “Kwa MutwaMkwava na
Mashujaa wengine” ambapo mtunzi anasema;
‘…Shujaa Mkwawa hujafa
waishi
Na sauti yako ingali
aushi
Nasikia
Katika mpwito wa umma
mapito
Nasikia
Katika nyimbo za watoto
Soweto
Za wanyonge wapingao
ubaguzi…”
Waafrika
wanaamini kuwa watu walio kufa wapo karibu na Mungu na wale walio hai humuomba
Mungu kupitia wale waliokufa. Hili linajidhihirisha kupitia urithishaji wa
majina pamoja na matambiko au kuomba
mizimu ya mababu inayofanywa na waafrika wengi katika maisha ya kila siku.
Dhana
ya uzuri na ubaya pia imejidhihirisha kama falsafa ya kiafrika hasa katika
shairi la 19 “Wimbo wa Moyo” linalopatikana katika “Kunga za Ushairi”. Mtunzi
wa diwani hii anadokeza kuwa uzuri au ubaya upo katika macho ya muonaji au anayeangalia,
anasema;
“…Nimeamua kukuimbia
leo
Jinsi wewe univutiavyo
Usooni tabasamu la
huba;
Cheko lako ukicheka
Huniambukiza furahayo
Dodo mbivu matitiyo
Ni sherehe ya macho
yaonayo
Na mikonayo yenye
mbinu
Kiuno cha minenguo
Na macho ya uchawi
Konyezo la moyo
uguswao
Hunitoa miayo ya hamu…”
Hii
ni dhahili kuwa aghalabu uzuri au ubaya wa kitu kwa waafrika unategemea na
mtazamo au mawazo ya muonaji. Hata katika jamii mtu anaweza kupenda au kukiona kitu
fulani kizuri na mwingine kukiona kitu hicho ni kibaya.
Pia
katika tamthiliya ya “Nguzo Mama” mwandishi ameonyesha falsafa mbalmbali ambazo
zimezoeleka na zinatumika sana na jamii ya kiafrika. Falsafa zinazojidhihirisha
katika tamthiliya hii, ambazo ni kama vile;
Dhana
ya ngoma na nyimbo, katika tamthiliya hii mwandishi ameonyesha namna ngoma na
nyimbo zinavyochukuliwa katika jamii nyingi za kiafrika. Ngoma na nyimbo
huchukuliwa kama ni dhana ambazo zinazochochea umoja na ushirikiano kwa jamii
wakati wa kufanya kazi na mara dhana hizi zinapokosekana kazi huzorota na hata
watu huvunjika moyo na kushindwa kufanya kazi, na mwisho hutawanyika. Mwandishi
“Penina Muhando” ametumia ngoma na nyimbo kama kichocheo cha kufanya kazi
miongoni mwa wanawake wa Patata katika kuinua Nguzo mama kama inavyojitokeza
katika ukurasa wa 44 na pia sehemu kubwa ya tamthiliya hii. Hivyo huu ni
uhalisia uliopo katika jamii za kiafrika hususani kwenye makabila mbalimbali,
ngoma na nyimbo huchukuliwa kama vichocheo na viashiria vya matukio ndani ya
jamii.
Dhana
ya mwanamke katika jamii, mwandishi Penina Muhando ameonyesha namna mwanamke
anavyochukuliwa na jamii. Suala hili mwandishi amelizungumzia sana katika
tamthiliya hii, kwani amewateua wanawake wa Patata namna wnavyojishughulisha na
kazi mbalimbali katika familia zao na hata katika kuinua Nguzo mama huku
akiwachora wanaume namna wanavyo wadharau wanawake kwa kushindwa kuinua Nguzo
mama. Lakini pia namna wanaume wanavyowatesa wake zao, mfano Bi. Pili namna
anavyojitahidi kuwahangaikia watoto wake huku mume wake akiwa ni mtu wa kunywa
pombe na pale anaporudi nyumbani huishia kumpiga mke wake. Jambo hili lipo
miongoni mwa jamii za kiafrika ambapo mwanamke anachukuliwa kama kiumbe duni
asiyeweza chochote mbele ya mwanaume na ndio mitazamo ya wanaume na wazee katika
familia nyingi za kiafrika,kwa mfano mtoto wa kike mara nyingi hutengwa na mtoto
wa kiume katika shughuli mbalimbali likiwemo suala la elimu. Kwa hiyo mwandishi
ameonyesha namna gani falsafa ya kiafrika inavyojidhihirisha juu ya
anavyochukuliwa mwanamke, tofauti na Ulaya na Asia ambapo mwanamke amepewa
nafasi kama mwanaume katika Nyanja zote
za kimaisha. Mwandishi katika ukurasa wa 36 anamuonesha Bi. Pili namna
alivyojishughulisha na kuuza pombe ili aweze kuwatunza watoto wake, lakini bado
anaonekana hafai mbele ya mume wake ambaye yeye kazi yake kubwa ni kuywa pombe
na kumtukana mke wake, Bwana Sudi anasema
“Kelele!Sasa mimi nitavaa nini.
Utakausha kwa moto hiyo nakwambia. Mimi nataka kurudi nilikotoka nimeacha pombe
kafiri. Unataka wenzangu wamalize? Kausha hiyo nguo kabla sijakupiga”.
Vile
vile kupitia riwaya ya “Mirathi ya Hatari” iliyoandikwa na C. G. Mung’ong’o
tunashuhudia falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika vipengele vifuatavyo
kama ifuatavyo;
Suala
la uhai na kifo, waafrika walio wengi mbali na kuamini kuwa vifo vingi
vinavyotokea katika jamii vina sababu zake ambazo huelekezwa katika Mungu na
uchawi au ushirikina. Haya yamezungumzwa na wanafalsafa wa kiafrika kama vile
Placide Temples na Samweli Mbiti. Katika riwaya hii hali hii inajidhihirisha
kupitia kifo cha mzee Kazumbe. Katika ukurasa (uk 37) inagundulika kwamba chanzo
cha kifo ni kulogwa, mwandishi anasema “Mwanangu, leo asubuhi nilikwenda kwa
mama Tumwene kuulizia kifo cha baba yako. Uganga unasema kuwa kifo chake
kimetokea si kwa mapenzi ya Mungu, ila kwa michezo ya binadamu wafaidio kuwaona
watu wakifa! Vile vile imesemwa mchezo haukwishia kwa marehemu wengine wetu
watafuata hivi karibuni”. Huu ni uhalisia katika jamii zetu mbali na uwepo wa
hospitali bado tunaamini nguvu za kiganga na kichawi.
Pia
suala la dini, kupitia mwanafalsafa John Samweli Mbiti ni dhahiri kuwa waafrika
wana dini zao tangu mwanzo mbali na ujio wa wakoloni ambao walileta ukristo pamoja na uislamu wao. Katika riwaya
hii mwandishi kupitia wahusika kama Gusto na mama yake (Nyamidze) ni wakristo
tena huwa wana kwenda kanisani katika (uk 29) baada ya Gusto kuoga na kuvaa ili
aende kanisani anamuuliza Nandi, “Hivi mama amekwenda wapi?” Nandi anajibu
“Amekwenda kanisani”. Ni usiku huo huo tu wa kucha jumapili Gusto alihudhuria
kikao cha wachawi mapangoni. Siku hiyo hiyo ya Jumapili mama yake Gusto
(Nyamidze) anaenda kwa mganga (uk 37) kwa mama Tumwene. Huu ni uhasilia katika
jamii zetu, matatizo yanapoikumba familia za watu mbalimbali miungu
hukimbiliwa. Uamini kuwa mtu akifa hujiunga na miungu.
Suala
la urithi, katika falsafa ya kiafrika tunaamini mzazi hasa baba anapofariki
huwaachia urithi watoto wake hasa wa kiume. Urithi huo ni pamoja na mali za
marehemu. Katika riwaya hii Gusto anarithishwa uchawi wa baba yake katika (uk
15) mwandishi anasema “Mwanangu na kuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa
ukiutumia vyema; bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo. Nakuachia
dawa zote na milki yangu katika mizungu ya sihiri”. Mirathi hii anaipokea Gusto
na baadaye inasababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo vya mama, dada,
na hata kipenzi chake Dina ambapo vifo vimetokea kama kisasi baada ya Gusto
kumtoa kafara mjomba wake Kapedzile. Suala hili la urithi lipo na linajidhihirisha
katika jamii zetu za kiafrika.
Kwa
kuhitimisha, tunaweza sema kuwa falsafa ya kiafrika imejikita hasa kuelezea
mfumo mzima wa maisha anayoishi mwaafrika na ukweli kuhusu fikra, mila,
utamaduni, na mienendo yake katika jamii. Kwa sasa falsafa ya kiafrika
imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na falsafa ya kimagharibi hususani suala zima la
utandawazi. Waafrika taratibu wanasahau mila na desturi zao na kwa kiasi
kikubwa kufuata na kuiga utamaduni na mwenendo wa maisha wa kimagharibi katika
masuala mbalimbali kama vile, mavazi, vyakula (vyakula vya asili kama vile
maboga, magimbi, viazi, pamoja na mihogo vina puuzwa kwa kiasi kikubwa na
kizazi cha wakati huu), suala zima la dini, mfumo wa elimu na afya vyote
vimebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzuka kwa utandawazi. Pia maendeleo
ya sayansi na teknolojia yamesababisha falsafa ya kiafrika kwa kiasi kikubwa
kupotea, mfano ngoma za jadi katika kizazi hiki zinazidi kupotea kutokana na
kuibuka kwa taaluma ya muziki kutoka katika iamii za kimagharibi.
MAREJEO.
Kahigi,
K.K., & Mulokozi, M.M. (1979). Kunga
za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzani Publishing House
Mbiti,
J. (1990). African Religion and
Philosophy. New York: Praeger Publisher
Muhando,
P. (1982). Nguzo Mama. Dar es Salaam:
Dar es Salaam University Press
Mung’ong’o,
C.G. (1977). Mirathi ya Hatari. Dar
es Salaam: Tanzania publishing House
Wamitila,
K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi
na Nadharia. Nairobi: Focus Publications
No comments:
Post a Comment